Magunia ya sukari. Picha/hisani

Share news tips with us here at Hivisasa

Mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini KRA imekata rufaa kupinga kuhifadhiwa kwa magunia elfu mia nane ya sukari katika bohari moja la kibinafsi.

Rufaa hii inajiri baada ya jaji Erick Ogola mnamo Januari nane kuagiza kampuni ya Darasa Investiment Ltd kuhifadhi tani laki nne za sukari katika bohari la J.B Maina badala ya mabohari ya bandari ya Mombasa.

Sukari hiyo inadaiwa kuagizwa kutoka nchini Brazil na kwa sasa bado iko kwa meli baharini  ikisubiri uamuzi wa mahakama kuu,kuhusiana na wapi itahifadhiwa.

KRA imekata rufaa hiyo kwa kusema kuwa mahakama haina uwezo wa kuagiza sehemu ambayo sukari hiyo inafaa kuhefadhiwa.

Kupitia wakili wao KRA, Kennedy Ogotto wameimbia mahakama kuwa watahitaji magari zaidi ya 150 ya kubebea mizigo kuweza kusafirisha sukari hiyo hadi katika bohari la J.B.Maina ambalo liko upambali wa kilomita sita kutoka bandari ya Mombasa.

Siku ya Jumatano, alisisitiza kuwa wanahofia usalama wa sukari hiyo iwapo itahifadhiwa katika bohari hilo,huku akisitiza kuwa huenda wakenya wakapoteza ushuru wa shilingi bilioni 2.5 iwapo sukari hiyo itaibiwa.

Ameongeza kuwa bohari hilo halijatimiza vigezo muhimu hitajika kwa kuambatana na kanuni za mabahari.

Kwa upande wa kampuni ya Darasa Investiment Ltd,kupitia wakili wao Fred Ngatia wameitaja hatua ya KRA kama njama ya kukandamiza uhuru wa wateja wake kwa kusema kuwa sheria inawaruhusu kuhifadhi sukari hiyo sehemu yoyote  waliochagua.

Ngatia amepuzilia mbali madai ya KRA kuwa bohari la J.B.Maina halijatimiza vigezo na kanuni za mabahari nchini,huku Ngatia akishikilia kuwa bohari hilo lina hudumu kwa kuambatana na sheria.

Kesi hii inajiri baada ya kampuni ya Darasa Investiment kuelekea mahakamani kupinga kutozwa ushuru na mamlaka ya KRA.

Ikumbukwe serikali ilikuwa imeondoa ushuru kwa uagizaji wa sukari kutoka mataifa ya nje.

Mahakama itatoa uamuzi wake Februari 1, 2018.