Gavana Hassan Joho akizindua vifaa vya kupambana na ugonjwa wa Chikukungunya.[radiorahma.co.ke]

Share news tips with us here at Hivisasa

Waziri wa afya Cleopa Mailu ameilaumu serikali ya kaunti ya Mombasa kwa kukosa kuripoti kwa serikali kuu visa vya ugonjwa wa Chikukungunya ulioanza mwishoni mwa mwaka jana.

Mailu amesema serikali kuu kupitia wizara ya afya ingeingilia kati kukabiliana na ugonjwa huo wa  chikungunya mapema endapo serikali ya kaunti ya Mombasa ingeripoti kwa serikali kuu kama kaunti nyingine zinavyofanya.

Akizungumza katika hoteli moja jijini Mombasa siku ya Jumanne, amewahimiza viongozi wote wa kaunti zote nchini kuripoti visa vya ugonjwa wa kuambukizwa ili serikali kuu iweze kuingilia kati na kuukabili kwa ushirikiano wa pamoja.

Ameilaumu serikali ya kaunti ya Mombasa kwa kuzembea katika kukabili ugonjwa huo kwa haraka,hatua aliyoitaja iliyochangia idadi ya wagonjwa kuongezeka.

Wakati huo huo ni kwamba baadhi ya wakaazi wa Mombasa wameonekana kutoridhishwa na huduma ya kukabiliana na maambukizi ya maradhi ya Chikungunya inayotekelezwa na serikali ya kaunti.

Katika mahojiano na mwanahabari huyu, baadhi ya wakaazi wamedai kuwa dawa hiyo ilikuwa ikipulizwa katika mitaa iliyo na barabara pekee huku sehemu zisizopita magari zikiwa bado hazijafikiwa.

Wakiongozwa na Hamis Juma wameongeza kuwa licha ya kunyunyizwa kwa dawa hizo bado ugonjwa huo unaendelea kuathiri wananchi. 

Alisema kuwa wananchi wengi waliathiriwa na ugonjwa huo hali aliyoitaja kudhofisha afya zao.

Ameitaka wizara ya afya kaunti ya Mombasa kuweza kukabiliana na magonjwa yoyote kwa haraka ili kuwakinga wananchi kuto athirika zaidi.

Wakati huo huo wakaazi hao wameeleza haja ya serikali ya kaunti kutafuta mbinu mbadala ya kukabiliana na ugonjwa huo kwani unyunyizaji dawa unaonekana kugonga mwamba

Kwa upande wake Salim Ali ametoa pendekezo la kuwepo na ukaguzi wa kina kwa wageni na bidhaa zinazotoka nje ya nchi ili kuzuia maambukizi ya magonjwa ya kigeni.

Ameitaja hatua hiyo  kama ambayo itasaidia katika kupungaza maambukizi ya magonjwa mengine zaidi kusambaa nchini.