Masanduku ya kura [Picha/ standardmedia.co.ke]

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Ripoti kamili ya zoezi la kuhesabiwa upya kwa kura za eneo bunge la Changamwe itatolwa Ijumaa katika mahakama kuu ya Mombasa.

Zoezi hilo lilianza wiki iliyopita na kumalizika siku ya Ahamisi katika katika jumba la  Public works eneo la Shimanzi.

Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani na aliyekuwa mgombea wa kiti cha ubunge kwa chama cha Jubilee Abdi Daib, ambaye anapinga ushindi wa mbunge wa sasa Omar Mwinyi.

Wakati wa kuhesabiwa kwa kura hizo Wanahabari jijini Mombasa walimepatwa na mshangao baada ya kuzuiliwa kushuhudia zoezi hilo.

Hii ni baada ya maafisa wa tume ya uchaguzi kusema kuwa wamepewa agizo la mahakama kuwazuia wanahabari dhidi ya kushuhudia zoezi hilo ambalo linafanyika katika kituo cha kuhesabia kura katika jumba la  Public works eneo la Shimanzi.

Wanahabari hao wakiongozwa na Samir Ali kutoka Radio Rahma wamekashifu hatua na kuitaja kama ukiukaji wa haki za wanahabari.

Akizungumza siku ya Alhamisi wiki iliyopita , baada ya kuzuiliwa mwanahabari Samir amewataka wakuu wa vyombo vya habari pamoja na vyama vya kutetea wanahabari kuingilia kati ili kuona kwamba haki za wanahabari hazikiukwi.

Wanahabari wengine waliozuiliwa ni Galgalo Bocha wa gazeti la Nation, Malemba Mkongo wa gazeti la The Star pamoja na wanahabari wengine kutoka media max, Baraka fm na idhaa zingine.

Maafisa wa Iebc walioko katika kituo hicho wanadai kuwa kuna agizo lilitolewa na mahakama kuu ya Mombasa la kuwataka waandishi kutofuatilia zoezi hilo.

Hata hivyo Maafisa hao wameshindwa kuonyesha agizo hilo la Mahakama jambo ambalo linaibua wasiwasi miongoni mwa waandishi kuwa huenda maafisa hao wanajaribu kuwafunga macho kuficha mambo fulani.

Uamuzi wa kuhesabiwa upya kwa kura hizo unajiri baada ya Daib kupitia wakili wake Gikandi Ngubuin kuwasilisha ombi hilo mbele ya Jaji Mwangi.

Gikandi alisema kuwa kumekuwa na makosa mengi kwenye baadhi ya fomu na nakala zingine zilizotumika kwenye uchaguzi huo wa Changamwe na kuitaka mahakama kuagiza kura hizo kuhesabiwa upya ili ukweli kubainika.

Daib aliiambia mahakama kuwa Mwinyi aliongezewa kura 262 katika uchaguzi huo wa Agosti 8.

Kulingana na fomu 35B iliyowasilishwa mahakamani, Mwinyi alipata kura 31,584 kinyume na kura 31,322 ambazo zilitumwa kwenye mtandao wa matokeo ya tume ya IEBC.

Akitoa ushahidi huo mbele ya Jaji Mwangi, Daib aliitaja hatua hiyo kama njama ya wizi.

“Huu ni wizi wa wazi uliofanyika katika vituo vingi eneo la Changamwe ili kumpitisha Omari Mwinyi,” alisema Daib.

Ushahidi wake ulionyesha kuwa kura zilizoharibika kulingana na Fomu 35B ni kura 494, kinyume na zile zilizotumwa kwenye mtandao wa IEBC ambao ulionyesha kura 1,120.

Daib alitilia shaka tofauti hiyo na kuitaja kama njama ya wasimamizi wa kura hizo kutekeleza wizi.

“Tofauti hii ni ishara kuwa uchaguzi huo haukuwa wa uwazi na huru,” alisema Daib.

Aidha, picha na nakala ya kifaa cha KIEMS zilizowasilishwa mahakamani zilionesha tarehe ya uchaguzi kuwa Januari 2, 2009 wala sio Agosti 8, 2017.

Daib pia alidai kuwa mawakala wake 25 walitimuliwa kutoka vituo vya kupigia kura kama vile kituo cha Shule ya msingi ya Bomu, Baraka Village na Shule ya msingi ya Chaani, miongoni mwa vituo vingine.

“Mawakala wangu wengi walifurushwa vituoni pasi sababu mwafaka. Hii ilikuwa ni mjama ya wasimamizi wa uchaguzi kutekeleza wizi wa kura,” alisema Daib.

Vile vile aliwasilisha mahakamani picha mbili za vijana waliokuwa wamebeba mfuko wa plastiki pamoja na begi zilizodaiwa kuwa na karatasi za kura zilizokuwa tayari zimetiwa alama, wakiingia katika kituo cha Chaani.

Daid alidai kuwa vijana hao waliruhusiwa kutumbukiza karatasi hizo kwenye sanduku la mbunge.

“Vijana hawa walirusiwa kutumbukiza karatasi hizo pasi kuzuiliwa na wasimamizi wa kituo hicho cha kupigia kura. Huu ni wizi wa wazi,” alisema Daib.