Share news tips with us here at Hivisasa

Polisi wa kupambana na machafuko kaunti ya Kisii waliazimika kutumia vitoa machozi dhidi ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Kisii baada ya ghasia kuzuka kufuatia uchaguzi wa viongozi wa chama cha wanafunzi. 

Machafuko hayo yalianza Ijumaa jioni pindi tu baada ya matokeo ya uchaguzi huo kutangazwa. 

Kwa mujibu wa Baadhi ya wanafunzi wasiotaka kutajwa, huenda kulikuwa na ubatilishaji wa matokeo hayo. 

"Huenda uongozi wa chuo kikuu ulichangia katika utoaji wa matokeo, Kama ulikuwa uchaguzi wa huru na wa haki hakungekuwa na machafuko," mmoja wao alisema. 

Hata hivyo msimamizi wa chuo hicho katika afisi ya kushughulikia wanafunzi hao, Bi Gladys Osoro alihimiza wanafunzi kujiepusha na fujo ya aina yoyote akisema katika kila uchaguzi lazima kuwe na mshindi na mshindani. 

"Hatufurahishwi tunapoona baadhi ya wanafunzi wanahusika na masuala ya fujo nyakati za matokeo ya uchaguzi kwani kuna mpango uliowekwa wakushughulikia masuala kama hayo ila sio kwa fujo," alisema. 

Kufuatia tukio hilo, mali yenye thamani isiyojulikana imeharibiwa na wanafunzi hao huku wengine wakipoteza bidhaa mbali mbali. 

Wanafunzi walilazimika kuhama kutoka chuo hicho na kukimbilia usalama wao huku chuo hicho kikisalia chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa polisi.