Mwenyekiti wa Kitaifa wa chama cha Sauti ya Wajane Kenya, Roseline Orwa, amekashifu serikali kwa kupuuza wanawake wajane akisema kuwa wajane nchini wanapitia shida ambazo zafaa kusuluhishwa na serikali husika.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubia waandishi wa habari katika Chuo Kikuu cha Kisii, alipohudhuria hafla ya kufungua rasmi tawi la chama hicho cha Sauti ya Wajane-Kenya, kiongozi huyo alisema kuwa idadi ya wanawake wajane nchini ni zaidi ya milioni nane.

Orwa alisikitikia viongozi wa kisiasa kwa kuwakandamiza na kuwawacha bila mwakilishi wowote wa kuwatetea bungeni.

Wakati uo huo, Seneta mteule kutoka Kaunti ya Kisii, Janet On'gera, aliapa kuwasilisha ujumbe huo mbele ya bunge la seneti ili kuhakikisha kwamba wajane wamewakilishwa na hata kupata mgao wa fedha katika bajeti ya mwaka ujao.

Kauli hiyo pia iliweza kuungwa mkono na mkewe gavana wa Kaunti ya Kisii, Elizabeth Ongwae, ambaye alisema atahakikisha kuwa muungano huo wa wajane umeendelezwa.

Bi Ongwae alisema wanawake wajane wamekuwa wakipitia mateso mbalimbali yanayoambatana na mila zilizopitwa na wakati.

Kongamano hilo linatarajiwa kufunguliwa katika kaunti zote humu nchini huku Kaunti ya Kisii ikiwa kaunti ya kumi kuanzisha muungano huyo.

Baadhi ya kaunti zilizoanzisha muungano wa wajane ni pamoja na Siaya, Embu, Kirinyaga, Meru, Migori, Homabay, Nyandarua, Kisii na Nyamira.