Article Image
MOMBASA

Raia kumi wa Pakstani wazuiliwa korokoroni kwa muda wa siku kumi zaidi.

Osman Suleiman

Raia wa Pakstani waliokamatwa jijini Mombasa. [Picha/ Osman Suleiman].

Mahakama ya Mombasa imeagiza kuzuiliwa kwa muda wa siku kumi zaidi kwa raia kumi wa Pakstani wanaodaiwa kuwa humu nchini kinyume cha sheria.

Raia hao walitiwa mbaroni siku ya Jumatano katika maeneo tofauti jijini Mombasa.

Aidha, wanakabiliwa na madai ya kuendesha biashara haramu humu nchini.

Akitoa uamuzi huo hakimu Juliet Kassam,amesema kuwa washukiwa hao wazuiliwe kwa muda wa siku kumi ili uchunguzi dhidi ya kukamilika.

Aidha,ameagiza kesi hiyo kutajwa mbele yake mnano Januari 19 mwaka huu.

Uamuzi huu unajiri siku chache baada ya afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa kutaka kuzuiliwa korokoroni raia kumi wa Pakistani kwa muda wa siku 10 zaidi hadi uchunguzi utakapomalizika.

Ombi hilo liliwasilishwa mbele ya Hakimu Juliet Kassam na naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka tawi la Mombasa Alexendra Muteti.

Muteti anataka washukiwa hao kuziliwa korokoroni ili kutoa fursa kwa maafisa wa usalama kukamilisha uchunguzi wao.

“Tunataka muda zaidi maafisa wa upelelezi wamalize uchunguzi wao kabla ya kufunguliwa mashtaka kwa washukiwa hao,” alisema Muteti.

Muteti alisema kuwa muda huo utawapa fursa ya kubaini iwapo washukiwa hao wamekuwa humu nchini kwa zaidi ya miaka minne.

“Kuna tetesi kuwa washukiwa hawa wamekaa kwa muda wa miaka minne humu nchini na tunataka kuchunguza iwapo ni ukweli,” alisema Muteti.

Aidha, Muteti alisema kuwa uchunguzi huo utabaini iwapo washukiwa hao wamekuwa wakifanya biashara mbali mbali bila vibali mwafaka.

Alisema kuwa uchunguzi huo aidha utaweka wazi iwapo washukiwa hao wamekuwa wakikwepa kulipa ushuru kwa taifa la Kenya.

Report Story