Picha ya mchezo wa bahati nasibu maarufu kamari. [premiercasinohire.com]

Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali inatakiwa kupiga marufuku michezo yote ya kamari maarufu kama bahati nasibu, inayoendelezwa humu nchini ili kuokoa vijana na jinamizi hilo.

Akizungumza siku ya Jumanne, mwenyekiti wa baraza la Maulamaa na Wasomi wa Kiislamu la KAULI, Sheikh Badru Khamis alisema vijana wengi wanakimbia masomo kwa ajili ya kujipatia pesa za haraka zinazotokana na michezo hiyo ya kamari na bahati nasibu.

Aliitaja michezo hiyo kama inayotatiza shughuli za masomo,kwa kusema kuwa watoto wengi ufikiria jinsi ya kucheza kamari badala ya kuzingatia masomo shuleni.

Aliongeza kuwa kamari zimechangia pakubwa kuongezeka kwa wiziri hasa kwa vijana wadogo katika sehemu mbali mbali za taifa.

Jijini Mombasa mitaa ya Bombolulu, Kongowea na Likoni imeonekana kuwa na mitambo hiyo kwa wingi.

Itakumbukwa kuwa katika kaunti ya Kilifi vijana wawili wamewahi kujitoa uhai hivi karibuni kutokana na kushindwa kwenye michezo hiyo.

Na katika kaunti ya Kwale idara ya usalama imeanzisha msako wa kuzifunga maskani za kuchezea kamari wakiitaja  michezo hiyo kuwa kinyume cha sheria .

Akizungumza na wanahabari afisini mwake, mkuu wa polisi eneo la Matuga  Japhet Kibuga amesema kuwa  mchezo wa kamari umeathiri  vijana kwa kiwango kikubwa mno, hatua inayowafanya  baadhi yao kujiingiza katika maswala ya wizi ili kutafuta pesa za kuchezea kamari.

Aidha alidokeza kuwa kwa sasa wametia mbaroni zaidi ya wamiliki 10 wa mchezo huo na tayari wamewafikisha mahakamani ili wafunguliwe mashtaka dhidi yao.

Msako huo ulitekelezwa katika maeneo ya Tiribe, Maganyakulo, Tiwi, Waa na Kombani baada ya agizo la Waziri wa Usalama wa ndani Fred Matiag'i kutaka maskani zote za kamari kufungwa.

Siku ya Ijumaa waziri wa Usalama wa ndani na kaimu katika Wizara ya Elimu aliamuru kufungwa kwa mabanda yanayochezesha kamari nchini.

Baada ya agizo hilo la waziri oparesheni hiyo lilianzishwa katika maeneo ya Kericho na Ongata Rongai ambapo mitambo 78 ilipatikana na watu 15 kushikwa wakiendeleza biashara hiyo.

Msemaji wa wizara ya usalama wa ndani Mwenda Njoka ameeleza kuwa oparesheni hiyo itaendelezwa kote nchini.