Mwenyekiti wa tume ya ardhi nchini.Mohammed Swazur. [nation.co.ke]

Share news tips with us here at Hivisasa

Tume ya ardhi nchini imekanusha kuwepo njama ya unyakuzi wa ardhi ya makavazi ya kitaifa ya Fort Jesus jijini Mombasa.

Mohamed Swazuri ambaye ni mwenyekiti wa tume hiyo, anasema ukuta unaojengwa kuzunguka makavazi hiyo,ni kwa juhudi za kuhifadhi mazingira na wala sio unyakuzi wa ardhi kama inavyodaiwa.

Akizungumza jijini Mombasa katika maeneo ya makavazi ya  kitaifa ya Fort Jesus jijini Mombasa siku ya Jumanne, amesema kuwa wao kama tume wanaunga mkono mradi huo unaoendeshwa na serikali ya kaunti kwa ushirikiano na mamlaka ya kusimamia turathi na makavazi ya kitaifa.

Swazuri alisema anaupongeza ujenzi wa ukuta huo,licha ya kusema kuwa hawakushirikishwa wakati mradi huo ukianza.

Kauli hii inajiri Siku chache baada ya tume ya kitaifa ya ardhi nchini NLC kuishauri taasisi ya makavazi nchini kusitisha mara moja ujenzi wa ukuta wa kukinga makavazi ya Fort Jesus kutokana na mawimbi makali ya bahari tume hiyo imeiidhinisha taasisi hiyo kuendeleza ujenzi huo.

Swazuri amesema kuwa hatua ya kuunga mkono mradi huo sasa, unajiri baada ya kuwapo kwa mazungumzo na taasisi hiyo pamoja na serikali ya kaunti hiyo dhidi ya madai kuwa taasisi ya makavazi haikuwa inafuata sheria za ardhi kutekeleza shughuli hiyo.

Aidha ametaja unyakuzi wa ardhi ya umma kukithiri zaidi hasa msimu wa siasa kwenye kaunti za ukanda wa Pwani pamoja na zile za maeneo ya ukambani na kuonya walio na nia hiyo kuwa watakabiliwa kisheria.

Kwa upande wake mwenyekiti wa taasisi ya makavazi ya kitaifa Mzalendo Kibunja amesisitiza kuwa ujezi wa ukuta huo utatekelezwa kama ilivyo pangwa huku akipuuza madai yaliobuliwa kuwa taasisi hiyo inatumia ardhi zaidi na ile iliyostahili ni potovu.

Ameongeza kuwa ni jukumu lao la kukinga makavazi hasa yanayopakana na fuo za bahari kutokana na mawimbi makali ya bahari.

Itakumbukwa kuwa wiki iliyopita gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Ali Joho alipinga ujenzi huo akisema kuwa taasisi ya makavazi ilichukua ardhi zaidi ya Ekari 2 na kusema kuwa ujenzi wa ukuta huo unahatarisha maisha ya viumbe vya baharini.