Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Naibu wa rais William Ruto ataka vyama tanzu vya muungano wa Jubilee pamoja na kile cha Cord kuungana ili kuwe na chama kimoja katika kila muungano.

Akihutubia waumini wa kanisa la Kianglikana katika uga wa Gusii kwenye hafla ya kutawazwa askofu mpya katika Diosisi ya Kisii John Orina, Ruto alisema kuna umuhimu wa taifa hili kuungana ili wananchi wasiweze kugawanywa katika misingi ya kikiabila.

"Hii mambo ya kila mtu kuleta chama chake cha kikabila, cha ukoo haina msingi wowote, kwa hivyo sisi kama Jubilee tumeamua tuungane kwa pamoja na vyama tanzu kutoka URP, TNA na ile 'Basi' ya Kiraitu kwa hivyo tunahimiza wale wenzetu katika upande wa Cord kufanya vivyo hivyo," alisema Ruto.

Kiongozi huyo alisema kama viongozi serikalini watahakikisha kuwa siasa ya taifa hili iko katika misingi ya sera wala sio kikabila kama inavyoshuhudiwa.

"Tunataka siasa za nchi hii kuenezwa katika misingi ya sera wala sio kikabila kama tunavyoshuhudia nchini, hakuna mkenya yeyote aliyezaliwa kimakosa kutoka katika kabila flani," aliongeza Ruto.

Sherehe hiyo iliandaliwa na kanisa la kianglikana  ikiongozwa na askofu mkuu wa kanisa hilo humu nchini, David Wabukala.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na wale wa kaunti ya Kisii.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni, mkewe naibu rais, Rachael Ruto, Gavana wa Bungoma Ken Lusaka, mbunge wa Nyaribari Chache Richard Tong'i.