Afisa wa shirika la Kenya National Alliance of Street Vendors and Informal Traders (KENASVIT) Rosemary Kimani ameiomba serikali ya kaunti ya Kisii kurekebisha sheria za wafanyibiashara wadogo wadogo ili walipe ushuru kwa mwezi badala ya kulipa kwa siku.
Akizungumza katika mkahawa wa Storm hotel mjini Kisii wakati wanachama wa shirika hilo walikuwa wanapokezwa mafunzo ya jinsi watakavyojiinua kupitia biashara zao, Kimani aliomba serikali ya Kaunti kupunguzwa ushuru kutoka shillingi 40 kila siku na kuomba wafanyibiashara kujengewa vibanda ili kuzuia hasara ambayo husababishwa na mvua inaponyesha na hata vumbi wakati wa kiangazi.
“Changamoto ambazo wafanyibiashara wadogo wadogo hupitia ni kunyanyaswa na maafisa wa kaunti kwa kufurushwa kutoka mahali wanapouza. Naomba serikali iwatafutie mahali pazuri na kuwajengea,” alisema Kimani.
“Naomba ushuru pia ipunguzwe na iwe inalipwa kwa kila mwezi kwa wafanyibiashara hawa wadogowadogo ili wajiimarishe na kujiendeleza kimaisha,” aliongeza Kimani.
Kwa upande wake mwenyekiti wa shirika hilo katika kaunti ya Kisii Evans Mogunde naye aliomba serikali kujali maslahi ya wafanyibiashara hao wadogo wadogo ili kujiendeleza kwa kuwapunguzia gharama ya ushuru.