Share news tips with us here at Hivisasa

Wabunge wa Pwani wamehimizwa kubuni mradi sawia na ule wa Shirika la Huduma ya Vijana kwa taifa (NYS) katika maeneo bunge yao ili kuwaondoa vijana mtaani.

Afisa wa nyanjani wa shirika la kijamii la ‘Kenya Community Support Centre’ Mwalimu Rama, alisema kuwa miradi kama hiyo ina umuhimu Pwani kwani itasaidia kwa kiwango kikubwa kuzuia vijana wengi kujihusisha na maovu.

Rama alisema kuwa iwapo Wabunge watatenga fedha kutoka kwa hazina ya ustawi wa maeneo bunge (CDF) na kuidhinisha miradi mbalimbali ya vijana, basi wengi watanufaika na hazina hiyo.

Kiongozi huyo wa vijana katika Ukanda wa Pwani aliwashinikiza Wabunge kupigania fedha zaidi kwa hazina hiyo ili wapate mgao unaofaa na utakaowakimu vijana mashinani.

“ Tunawaomba wabunge wetu wa pwani kutumia fursa hii na kuomba fedha zaidi katika hazina zao za CDF ili kuwasaidia vijana na jamii katika kubuni nafasi za ajira sawia na mradi wa Shirika la vijana wa taifa NYS,” alisema Rama.

Rama aliwasihi vijana kutopuuza mradi huo na badala yake washiriki kikamilifu katika kazi hizo japo ni za msimu ila wapate fedha chache za kujikimu kimaisha.