Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Vuguvugu la Mombasa Rebublican Congress, MRC, sasa sasa limijitokeza na kuanza malengo ya kuwahimiza wenyeji wa Pwani kuishi kwa amani na kujiandikisha katika kupiga kura kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Wakiongea kwenye mkutano mmoja wa hadhara, wanachama hao, wakiongozwa na Rashid Mraja wamesema kundi hilo litahakikisha kuwa wanachana wao watashiriki katika uchaguzi na pia kuwahimiza wakazi kujiandikisha.

Mraja alidokeza kuwa yuko tayari kutoa hamasisho kwa vijana wengine ambao walikuwa na mtazamo hasi hapo awali baada ya mawazo potovu ya kundi hilo na kusema kuwa sasa ni wakati wa kuja pamoja na kuungana kama jamii ili kusaidia kizazi na kuendeleza nchi.

“Tupo tayari, iwe ni kwenye mikutano ya hadhara, kwenye hafla za matanga kwenye makongamano ya harusi kuwahamasisha wenyeji umuhimu wa kuishi pamoja na umuhimu wa kujisajili kama mpiga kura kwenye eneo unaloishi,” alisema kiongozi huyo.

Kundi la MRC limekuwa na mitazamo potovu ya kutaka kuitangaza Kaunti ya Mombasa kuwa si Kenya tangu uchaguzi wa 2007 na uchaguzi mkuu wa 2013, ambapo waliwachochea wenyeji kutochukua kura wala kuepuka kabisa kushiriki kwenye shughuli nzima ya kupiga kura.

Hatua hiyo ya kundi hilo itapokelewa na viongozi wa kisiasa kwa njia nzuri baada ya wengi kuhisi kuwa kundi hilo lingezua ghasia kwenye uchaguzi mkuu ujao.