Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu spika wa bunge la kaunti la Nyamira Andrew Magangi ameishtumu serikali ya kitaifa kwa madai ya kujaribu kuizuia kamati ya bajeti dhidi ya kutekeleza miradi fulani.

Akihutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumatatu, Magangi alisema kuwa serikali ya kitaifa ilikuwa imewazuia washiriki wa michezo kusafiri nchini Rwanda ili kushiriki katika michezo mbalimbali ya kimataifa ya Afrika iliyong'oa nanga tarehe 6 Disemba, kwa madai kuwa kushiriki katika michezo hiyo hakuongezi faida yoyote kwa wananchi.

"Ni jambo la kushangaza kuwa serikali ya kitaifa iliamua kuwazuia washiriki wa michezo kutoka bunge la Nyamira, michezo ambayo tayari imeng'oa nanga nchini Rwanda," alisema Magangi.

Magangi aliongezea kuwa hatua hiyo ya serikali ya kitaifa kuwazuia wakilishi wa wadi kushiriki katika michezo hiyo ni njia mojawapo za kukandamiza ugatuzi.

"Mbona wizara yakitaifa ya fedha iliidhinisha kushiriki kwa maseneta na wabunge kwenye kongamano hilo la michezo Rwanda na kuwazuia washiriki halisi? Kwa kweli hii ni mojawapo ya njia za kukandamiza ugatuzi nchini," alihoji Magangi.