Share news tips with us here at Hivisasa

Kamishena wa kaunti ya Kisii Chege Mwangi amewaonya wanachama wa polisi jamii wa kaunti hiyo dhidi ya kuchukua sheria mikononi mwao kwa kuwasumbua wananchi.

Kulingana na kamishena huyo, hakuna sheria inamruhusu mwanachama wa polisi jamii kumchapa mkaazi mwenzake anapokosa bali kazi yao ni kuwajulisha maafisa wa polisi ili kumtia mbaroni mshukiwa.

Mwangi alisema kazi ambayo wanachama hao wanafaa kufanya ni kushirikiana na maafisa wa polisi kuimarisha usalama katika vijiji mbalimbali.

Akizungumza siku ya Jumatatu mjini Kisii, Mwangi aliwaonya wanachama wanaochukua sheria mikononi mwao na kuwaomba kushirikiana na polisi kuleta usalama vijijini ila si kuwatesa wananchi wanapokosa.

“Hakuna mwanachama anaruhusiwa kumchapa mkaazi mwenzake ikiwa mkazi amekosa, bali julisha maafisa wa polisi ili atiwe mbaroni,” alisema Chege Mwangi

Aidha, kamishena huyo alifutilia mbali uchaguzi wa wanachama hao katika eneo bunge la Bochari na kusema kuwa wanachama wa polisi jamii wanastahili kuchaguliwa na wananchi kulingana na katiba kando na kuchaguliwa na machifu.

Pia Mwangi aliagiza uchaguzi huo kurudiwa na kufanywa na wananchi na kusema kuwa wale watachaguliwa hawafai kuwatesa wananchi kamwe kwani hiyo ni hatia na watakapofumaniwa wakikiuka sheria hiyo watachukuliwa hatua kali ya kisheria.

Mkuu wa polisi katika kaunti hiyo Simon Kiragu, alisema kuwa wanachama ambao watachaguliwa hawatalipwa bali kazi hiyo ni ya kujitolea kwa ihali.