Kamishena wa tume ya kuajiri walimu nchini Teachers Service Commission (TSC) Albert Keraba amewataka walimu wote wakuu wa shule mbalimbali nchini kutia sahihi kandarasi ya utendakazi wao jinsi tume hiyo ilivyoagiza hapo mbeleni.
Akizungunza katika mkutano wa walimu wakuu kaunti ya Nyamira, mkutano ambao uliandaliwa katika shule ya upili ya Kebirigo, Keraba aliwataka walimu wakuu kujaribu kila wawezalo kuhakikisha wametia sahihi kandarasi ya utendakazi ili kuleta uwazi na kuinua viwango vya elimu.
“Naomba walimu wakuu kuhakikisha yale yaliyoagizwa na tume ya TSC yamefuatwa na kufanywa ili tuwe na utaratibu katika kazi zetu tunazozifanya kielimu,” alisema Keraba.
Wakati huo huo, Keraba alikanusha madai ya vyama vya walimu, KUPPET na KNUT kuwa hawakuhusishwa katika maeleawano ya kutia sahihi kandarasi za utendakazi kwa walimu nchini.