Serikali ya kaunti ya Nyamira imetenga shillingi millioni 40, pesa zitakazotumika kununua magari ya kuzima moto.
Akihutubu nje ya afisi kuu za serikali ya kaunti ya Nyamira wakati wa kuwapokea wataalam wa kuzima moto kutoka marekani, gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama alisema kuwa serikali yake imeweka mikakati ya kuhakikisha mikasa ya moto inathibitiwa.
"Nimefurahi kwamba watu wetu watapokea mafunzo ya kuthibiti mikasa na tayari tumetenga shillingi millioni 40 ili kununua magari ya kuzima moto na ni ombi langu kuwa watakaopokea mafunzo kuhakikisha kuwa watakuwajibika kwa haraka ili kuthibiti mikasa," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha alisema kuwa magari hayo yatatumwa kuhudumu katika kaunti zote ndogo za kaunti ya Nyamira, huku akiwataka wakazi wa kaunti ya Nyamira kuwa na subira serikali yake inapoweka mikakati ya kutekeleza ahadi zake.
"Tutatuma magari matano katika kila kaunti ndogo ili kuthibiti mikasa katika maeneo hayo, na hii hatua ni miongoni mwa zile ahadi serikali yangu iliwapa wananchi na ndio maana nawaomba wananchi kuwa na subira ili kutupa nafasi ya kutekeleza miradi mbalimbali," aliongezea Nyagarama.