Baada ya kumwangazia mwanafunzi Natasha Moraa tarehe 17 February 2016, hapo jana mwanadada huyo alipata fursa ya kujiunga na shule ya kitaifa ya wasichana ya Nyabururu.
Natasha Moraa kutoka kijiji cha Bomatara, wadi ya Marani kaunti ya Kisii aliyejizolea alama 357 kutoka shule ya msingi ya Kisii alishindwa kujiunga na shule ya kitaifa ya Chogoria kwa sababau ya kutomudu karo.
Furaha mpwitompwito zikiandamana na unenguzi wa viuno ndiyo iliyokuwa taswira wakati wakujiunga kwake na shule ya wasichana ya Nyabururu.
Natasha aliyeabiri gari la Mwakilishi wa Wanawake Mary Otara alishindwa kuyazuia machozi ya furaha na kutoamini macho yake kuwa amefika Nyabururu.
Natasha amefadhiliwa na mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kisii Mary Otara ambaye alimlipia karo ya shilingi elfu themanini na nane ili kugharamia masomo yake.
Awali pia Natasha alikuwa amepokezwa cheki ya shilingi 27,788 na gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae.
Kupitia kwa msemaji wa Otara, alidokezea vyombo vya habari kuwa karo hiyo itakuwa inalipwa kila mwaka iwapo tu Natashasha atatia fora masomoni.
Akizungumza na wanahabari nje za afisi za shule hiyo Moraa ameahidi kutia bidii na kuwa mwanahabari baada ya kidato cha nne.
“Leo niko katika shule ya kitaifa ya Nyabururu, furaha yangu sitaweza kuelezea. Niko hapa kwasababu ya Mbunge Mary Otara pamoja na gavana vilevile na wasamaria wema," alisema Moraa.
"Na nitangara kimasomo katika shule hii. Sasa imewezekana kwamba niko shuleni, nitafanya bidii na nitakuwa mwanahabari wa runinga hivi karibuni,” aliongeza Moraa.