Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kamishina wa kaunti ya Kisumu John Elung’ati ametoa wito kwa Machifu na Manaibu wao kutumia nafasi yao katika jamii kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kujiandikisha kama wapiga kura.

Akizungumza katika kambi ya Chifu eneo la Nyabera jijini Kisumu, Elung’ati amesisitiza kuwa kuna vitambulisho vingi vya kitaifa ambavyo vimesalia katika afisi za Machifu.

Hivyo basi ipo haja ya kuhamasisha hasaa vijana kuhusu umuhimu wa stakabadhi hiyo na kuwashauri wafike katika afisi husika wajitwalie vitambulisho hivyo.

"Vitambulisho vya watu wengi vimesalia kwenye afisi za Machifu na afisi zingine za usajili wa watu kwa muda bila wenyewe kuchukua," alisema Elung'ati

"Ila wakati huu ni muhimu kwa kila mmoja kutambua kuwa ni muhimu kuwa na kitambulisho ndipo upate kuchukua kura utakayoitumia kwenye uchaguzi wa mwaka mkuu ujao,'' aliongeza Elung'ati.

Akijibu swala kuhusu kudorora kwa hali ya usalama hasaa maeneo ya Kolwar na Kajul, Elung’ati amesisitiza kuwa idara husika zinajizatiti kuhakikisha kuwa usalama unaimarisha na wahusika wa visa vya uhalifu wanakabiliwa kwa mujibu wa sheria.