Katibu wa chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini KNUT katika kaunti ya Mombasa Dan Aloo amemkosoa vikali waziri wa elimu nchini Fred Matiang'i kwa kutangaza kutenga shilingi bilioni 16 za ujenzi wa vyuo vya kiufundi.
Kulingana na Aloo, serikali ingefaa kuangazia maslahi ya walimu kwanza kutokana na kile anachosema kuwa serikali imekuwa ikikosa kuwalipa nyongeza ya mishahara na marupurupu yao ya asilimia 50 na 60 waliyokuwa wakidai.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Aloo alisema kuwa japo mpango huo una manufaa kwa wanafunzi watakaokosa kujiunga na vyuo vikuu, watafaidika na vyuo vya kiufundi ili kuwaondoa maskani lakini walimu pia wanafaa kuangaziwa.
“Tunashangazwa kuona serikali ikitangza kutoa shilingi bilioni 16 kujenga vyuo vya kiufundi na ilhali walimu bado mpaka sasa wanangoja ahadi waliyopewa na serikali, na iwapo itazidi kutulaghai, basi mpango ni ule ule wa mgomo,” alisema Aloo.
Aloo aliwahimiza wanafunzi kutolaghaiwa na serikali, na badala yake kusikiza mwongozo kutoka kwa viongozi wao wa chama chao cha KNUT kuhusiana na maswala ya kuishinikiza serikali kutimiza ahadi waliyowapa walimu.
Waziri Matiangi alisema kuwa vyuo hivyo vitatoa nafasi kwa zaidi ya wanafunzi 290,000 kote nchini waliokosa alama za kujiunga na vyuo vikuu na kuendelea na masomo yao.