Zaidi ya vijana elfu moja wamendamana mjini Mombasa na Malindi kufuatia ongezeko la baadhi yao kufariki kutokana na utumizi wa dawa za kulevya wakidai kuchangiwa pakubwa na ukosefu wa ajira.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa vijana eneo la Kisauni Maxwell Masai, vijana hao wamesema kuwa zaidi ya vijana 50 wamefariki katika kipindi cha mwaka mmoja kutokana na utumizi wa kokeni na Heroini.
Akizungumza mjini Mombasa wakati wa maandamano hayo, Masai alisema kuwa lazima vijana kujitokeza na kipinga vikali utumizi wa mihadarati ili kaunti hiyo iwe salama na vijana waathiriwa wanasuliwe kutoka janga hilo.
“Tunawaomba vijana wa eneo hili kujtenga na utumizi wa dawa za kulevya na kujiendeleza kwa miradi mbalimbali ya kimaendeleo na tunashinikiza idara husika za serikali kuingilia kati swala hili ili kuwaokoa vijana wengi,” alisema Masai.
Kwengineko kiongozi wa vijana katika eneo la Shella mjini Malindi Mohammed Salim, amewalaumu viongozi wa kaunti ya Kilifi pamoja na serikali kuu kwa kupuuzilia suala hilo na kuchangia idadi kubwa ya vijana kuathirika katika eneo hilo la Malindi na ukanda wa Pwani kwa jumla.
Wakati huo huo wameikosoa ziara ya gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho mjini Malindi wakisema kuwa viongozi kama hao wanapaswa kutatua suala hilo badala ya kupiga kampeni za kisiasa mjini humo.