Onyo kali imetolewa kwa yeyote atakayepatikana akiharibu vifaa vya kusambaza nguvu za umeme katika maeneo tofauti ya Kaunti ya Mombasa.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya kusambaza nguvu za umeme kaunti ya Mombasa Ezekiel Mwaolala amesema kuwa tabia hiyo inapaswa kukomeshwa haraka iwezekanavyo ikizingatiwa kuwa ni ukiukaji wa haki za wananchi sawia na kwenda kinyume na maagizo ya kikatiba.
Haya yamejiri baada ya wakaazi wa Mombasa kuelekeza lawama zao kwa kampuni hiyo ya kusambaza umeme kutokana na kukithiri kwa tatizo la kupotea kwa nguvu za umeme.
Akizungumza siku ya Jumatano katika eneo la Old Town ambapo shughuli za kukarabati soko hilo zinaendelea baada ya agizo la Rais Uhuru Kenyatta la kukarabati soko hilo, Mwaolala alisema kuwa uhalifu huo wa kukata nyaya za kupitisha nguvu za umeme umekuwa ukitekelezwa na baadhi ya vijana wanaokisiwa kutumia aina flani ya unga unaopatikana katika transfoma kama mihadarati.
“Tayari uchunguzi wa visa hivyo vya uharibifu wa bidhaa za kusambaza umeme unaendelezwa. Nawaomba wananchi kuwajibika katika kuripoti mtu yeyote anayetekeleza shughuli za umeme haswa katika milingoti bila ishara yoyote kutoka kwa kampuni ya kusambaza umeme,” alisema Mwaolala.