Share news tips with us here at Hivisasa

Hata baada ya idara ya usalama katika kaunti ya Mombasa kuzidisha juhudi za kutokomeza makundi ya kuwahangaisha wakaazi katika eneo bunge la Kisauni, sasa inaidaiwa kuwa vijana sugu wameanza harakati za kuwatia hofu.

Vijana hao maarufu kama 'Wakali kwanza' wamewashambulia wakazi juzi wakati wa jioni, ambapo walikuwa wakiingia katika nyumba za makaazi pamoja na maduka ya kuuza bidhaa na kuchukua pesa kutoka ka wamiliki wa maduka hayo.

Akiongea kwa niaba ya wakazi hao Mzee Mwinyi Aboud, alisema kuwa vijana hao walionekana wakiwalenga wenye magari na wakazi ambao wanatoka msikitini kusali.

Amesikitikia hali hiyo na kusema kuwa huenda kundi hilo limerudi makusudi na wanashuku kuwa vijana hao wanafadhiliwa na baadhi ya wanasiasa ambao wanahisi hofu ya kupoteza kura za wenyeji hasa wale wa kutoka katika maeneo ya mashambani.

“kinachotusinya sisi ni vile vijana hao wanajitokeza wakati ambapo watu wanaendelea kuchukua vitambulisho pamoja na kadi za kupiga kura, hii ni mbinu ya baadhi ya wanasiasa ambao wanataka kuwatia wakazi hofu kwa kusudi la kutaka kuepuka kupiga kura ifikapo mwaka ujao,” alilalama Fatma, mkazi wa eneo la Kisauni.

Hata hivyo watu wa eneo hilo wanasubiri kusikia kutoka kwa kamishina wa kaunti hiyo Nelson Marwa ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kuyakabili makundi hayo haramu.