Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko amewataka wakazi wa kaunti hiyo kusitisha mpango wa kuhama maeneo yao na kujisajili kama wapiga kura katika maeneo mengine kwa kupewa pesa.

Akiwahutubia wakazi wa Likoni siku ya Jumatatu, Mboko alisema kuwa njia pekee ya kubadilisha uongozi wa nchini na katika maeneo ya ubunge na hata ngazi za wadi ni kwa kupiga kura mahali unapoishi, hatua aliyosema italeta uongozi bora.

Mboko alisema kuwa kuna haja ya wakazi kufahamu kuwa kuhama katika kituo kimoja hadi kingine kujisajili kama mpiga kura ni haki ya kidemkrasia lakini hakutasaidia kubadilisha uongozi duni wa eneo mkaazi analoishi.

Mboko aliahidi kuzuru mashinani kuwashinikiza wakazi kuhafamu umuhimu wa kujisajili kama mpiga kura katika maeneo wanamoishi ili mkazi aweze kushiriki moja kwa moja katika uchaguzi mkuu ujao.

Aliwahimiza kujitenga na watu wanaowapa pesa ili kuhamia maeneo mengine.

“Ninapanga kuzuru mashinani kuwaelimisha wakazi kufahamu umuhimu wa kujisajili kama wapiga kura katika maeneo wanamoishi, na kuwaonya kutowakubali walaghai kuwadanganya kwa kuwapa pesa ili kuhama maeneo mengine kujisajili kabla muda uliowekwa na Tume ya IEBC Kuisha,” alisema Mboko.