Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mrengo wa Cord nchini umeishitumu serikali kuu kwa kushindwa kudhibiti kukithiri kwa ufisadi nchini, na badala yake kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kujiuzulu mamlakani.

Naibu Kinara wa chama cha ODM nchini Ali Hassan Joho amesema kuwa serikali ya Rais Kenyatta imesheheni wezi wa mali ya umma, na iwapo wafuasi wake watasalia madarakani, basi mali ya umma itaangamia kutokana na tamaa ya viongozi na maafisa wafisadi.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumapili, Joho alisema kuwa kutangazwa kwa taifa hili kuwa la tatu barani Afrika kwa kusheheni kwa kashfa za ufisadi kumedhihirisha wazi kuwa taifa hili linaangamia na huenda uchumi wa taifa hili ukaangamia zaidi.

Amesema kuwa hatua hiyo inaonyesha wazi kuwa serikali inafaa kuvunjwa na uchaguzi mkuu kufanywa mara moja ili mrengo wa Cord uchukue uongozi utakaobadilisha sura ya nchi.

“Hii ni aibu kubwa sana kwa taifa hili kuorodheshwa kuwa la tatu Afrika kwa kusheheni kashfa za ufisadi kutokana na tamaa za baadhi ya viongozi serikalini na maafisa wa umma," Alisema Joho.

"Kama mrengo wa Cord, tutahakikisha kuwa serikali  hii fisadi tumeibandua madarakani na kuongoza taifa hili kikamilifu,” aliongeza Joho.