Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Tume ya Maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC imeshinikizwa kumheshimu Kinara wa mrengo wa Cord Raila Odinga, kuhusu sakata ya fedha za dhamana ya mkopo wa Euro badala ya kumhujumu.

Mwenyekiti wa Kamati ya uhasibu wa fedha za umma katika kaunti ya Mombasa Fadhil Mwalimu, amesema kwamba hatua ya tume hiyo kumhujumu Raila kama aliyefuja fedha hizo kamwe sio sawa kikatiba na hatua hiyo huenda ikaleta mgogoro.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu katika mkutano wa kisiasa, Fadhil alisema kwamba tume hiyo inafaa kufanya uchunguzi kuhusu ripoti aliyoitoa Raila na iwapo wanamhitaji kuwasaidia kwa kuwapa ushahidi kuhusu sakata hiyo, basi wanahaki kumuita lakini sio kumdhalalisha.

Mwalimu alisema kwamba waliyotajwa katika sakata hiyo ndio wanaofaa kuchukuliwa hatua za kisheria na kueleza jinsi shilingi bilioni 140 zilivyotumika badala ya kuleta sinto fahamu kwa wananchi.

"EACC ni lazima imheshimu Raila Odinga kwani ndiye aliyechangia katika kuleta demokrasia. Akisema kuwa fedha zinatumiwa vibaya lazima mchunguze hilo badala ya kumdhalilisha. Sisi kama wanachama wa Cord hatutakubali hayo,” alisema Mwalimu.

Kauli yake imejiri huku afisa mkuu wa Tume ya EACC Halake Waqo akisema kwamba ameondoa agizo la kumkamata Raila.

Waqo alisema tume hiyo itaendelea na uchunguzi kisha baadaye wakimhitaji Raila, watamuita kuandikisha ripoti mbele ya tume hiyo.