Serikali ya kaunti ya Nyamira imefungua soko jipya katika eneo la Tombe wadi ya Manga ili kuimarisha biashara katika kaunti hiyo.
Soko hilo lilifunguliwa baada ya mapendekezo ya wakaazi na wafanyibiashara wa eneo.
Akizungumza siku ya Jumanne katika soko la Tombe wakati wa ufunguzi wa soko hilo Mwakilishi wa wadi ya Manga Peter Maroro alisema soko hilo litawanufaisha wengi.
aliongeza kusema kuwa serikali ya kaunti pia itafaidika pakubwa kwa kupata pesa za ushuru ambazo zitakusanywa katika soko hilo na kutumika kufanya maendeleo.
“Soko ambalo mlikuwa mnahitaji katika eneo hili limefika, sasa nyinyi fanyeni biashara ili muinue uchumi wa kaunti na taifa la Kenya,” alisema Maroro.
Soko hilo jipya litakuwa likifanya biashara zake siku mbili kwa wiki amabazo ni Jumanne na Alhamisi.
Wafanyibiashara nao walifurahia na kupongeza serikali ya kaunti kwa kuwakumbuka na kuwafungulia soko hilo.
"Sasa tutakuwa tukifanya biashara katika soko hili jipya na kujiendeleza kimaisha kwani wengi wetu tunategemea biashara hii ambayo tunafanya,” alisema Alice Kerubo, mwanabiashara.