Masomo ni kitu cha muhimu kwa kila mtu na ndio maana tunaambiwa kuwa elimu ni nuru ya maisha lakini kwa kijana mmoja, hiki sio kisa.
Abdul Mohamed wa miaka 21 aliamua kuanzisha biashara kuliko kuendelea na masomo. Mohamed aliacha shule ya upili ya county akiwa kidato cha pili mwaka 2010 kwa kuwa aliona masomo yamekuwa magumu na hivyo basi kubadili nia na kuanza biashara.
“Niliacha shule kwa vile nimeona masomo ni magumu na sikuweza kuendelea,” alisema Mohamed.
Kijana huyu pia alisema kuwa aliweza kupata ushawishi mkubwa kutoka kwa baadhi ya marafiki zake walioacha shule ambao kwa sasa wanafanya biashara ya bodaboda mjini Garissa.
“Kuna marafiki zangu ambao wameacha shule na wanafanya kazi ya bodaboda na wakanishawishi nijiunge nao badala ya kukaa nyumbani bila kufanya chochote,” alieleza kijana huyo.
Kwa sasa, anaendesha bodaboda yake binafsi na anfurahia maisha kwa kuwa anapata mapato mazuri ya kuweza kukidhi mahitaji yake binafsi na ya familia yake.
“Sasa hivi ninafurahia kazi yangu kwa vile inalisha familia yangu nami pia najikidhi kutokana na mapato yangu,” alisema
Mohamed anatoa wito kwa wanafunzi wote ambao wamo shuleni kujikaza kisabuni ili waweze kutimiza ndoto zao maishani.