Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Machifu na manaibu wao katika Kaunti ya Nyamira wamehimizwa kuwatia mbaroni watakaofumaniwa wakiendeleza ukeketaji wa wasichana.

Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa ukeketaji huendelezwa kwa kiasi kikubwa wakati wa likozo za Disemba, baada ya wanafunzi kufunga shule.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne mjini Nyamira, afisa mkuu wa watoto katika Kaunti ya Nyamira Samuel Sese alisema ofisi yake kwa ushirikaino na ofisi ya kamishena wa kaunti hiyo itachunguza wanaoendeleza shughuli hiyo iliyo kinyuma cha sheria.

Aidha, aliomba machifu na manaibu wao kujaribu kila wawezalo kuhakikisha kuwa ukeketaji umesitishwa katika kaunti hiyo.

“Watoto wasichana hawastahili kukeketwa na yeyote atakayepatikana atakabiliwa kisheria kwa kufungwa gerezani miaka mitatu na kutozwa faini ya Sh200,000,” alisema Sese.

Aliongeza, “Tayari tumeweka watu katika vijiji mbalimbali ambao watachunguza wale watakiuka sheria hiyo na kuwatia mbaroni.”

Afisa huyo aidha aliwashauri wazazi kuasi mila hiyo potovu.