Idara ya usalama kaunti ya Mombasa imewataka machifu na manaibu wao kueleza bayana kinachochangia kukithiri kwa visa vya uhalifu mashinani.
Kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa alisema kwamba maafisa hao tawala wanachangia hali ngumu ya idara ya usalama kuimarisha usalama wa kaunti hiyo kufuatia wengi wao kushindwa kuzuia kukithiri kwa visa vya uhalifu.
Marwa alisema vita dhidi ya wahalifu lazima vitaendelea hadi pale usalama wa kaunti hiyo utakapoimarika, huku akiwahimiza maafisa hao tawala kusaidia kuwakabili wahalifu badala ya kulaumiana na maafisa wa polisi.
"Tunataka machifu na manaibu wao kutueleza ni kwa nini wahalifu wanaongezeka mashinani katika maeneo yao na serikali inajitahidi kukabiliana nao, hii inaonesha kwamba baadhi yao wamezembea katika majukumu yao na kuchangia visa vingi vya uhalifu katika kaunti hiyo," alisema Marwa.
Kamishna huyo, ametoa onyo kali kwa maafisa hao tawala kuzidisha juhudi zao za kukabiliana na wahalifu,la sivyo hatua za kisheria dhidi yao zitachukuliwa kwa vile wengi wao wanaonekana kuzembea katika majukumu yao.