Mwakilishi wa wadi ya Sensi eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini kaunti ya Kisii amelahumiwa vikali dhidi ya kutotimiza ahadi zake.
Hii ni baada ya mwakilishi huyo Onchong’a Nyagaka kuahidi kuanzisha mradi wa maji katika sehemu mbalimbali za wadi yake zaidi ya miaka miwili iliyopita na hadi sasa hakuna mradi wowote wa maji umeanzishwa.
Wakaazi wa wadi hiyo wakiongozwa na Hesbon Kenguru na Irene Onchoke walimlahumu mwakilishi huyo kwa kukawia kutimiza ahadi zake.
Wakaazi hao pia wakatisha kutomchagua katika uchaguzi wa mwaka ujao ikiwa hatatimiza ahadi zake kabla ya wakati huo.
“Tuliahidiwa kuchimbiwa kisima katika eneo la Nyakeiri, maji ambayo yatatumiwa na wakaazi wa Chimo, Nyakeiri, Isambo, Moyare na lakini hakuna chochote kimefanywa hadi sasa,” alisema Kenguru.
Juhudi za kumtafuta mwakilishi huyo ili tupate usemi wake kwa swala zima la lalama hizo zilipofua dafu, alisema kuwa amemaliza mikakati ya kuanzisha kuweka miradi hiyo ya maji katika sehemu alizoahidi kabla ya mwaka huu kukamilika.