Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa kijiji cha Suberical mjini Naivasha wamejawa na wasiwasi baada ya mwili wa mwanamme mmoja kupatikana ukiwa umetupwa kando ya barabara.

Wafanyikazi wa kampuni za maua waliokuwa wakielekea kazini Jumatatu asubuhi, waliupata mwili huo unaodaiwa kuwa umeoza ishara kuwa ulikuwa umekaa eneo hilo kwa muda mrefu.

Mkazi mmoja Peter Kamau amesema kuwa mwanamme huyo mwenye umri wa makamo alikuwa na alama za kudungwa mara kadhaa kwenye kifua na shingo.

"Tumeona kuwa mwili huu una alama ya kudungwa na kisu kifuani na shingoni, huenda aliuawa kwingine na mwili wake kutupwa hapa," alisema Bw Kamau.

Na huko Karagita mjini humo, mwanamke mmoja, mama wa watoto wawili amepatikana akiwa amejitoa uhai mapema Jumatatu asubuhi.

Mkazi mmoja Joshua Ochieng' amesema kuwa mwanamke huyo alikuwa ameandika notisi ya kuonyesha sababu za kujitoa uhai ambayo ilisema kuwa hangeweza kuvumilia masaibu ya kukosa kazi.

Afisaa mmoja wa polisi ambaye alitaka jina lake kubanwa amedhibitisha matukio hayo na kusema kuwa uchunguzi umeanzishwa kwenye kisa cha kwanza.

Miili hiyo ilichukuliwa na kupelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya wilaya ya Naivasha huku watoto wawili wa mwanamke huyo wakipelekwa katika makao ya watoto iliyoko karibu na eneo hilo.