Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mashirika ya kijamii katika eneo la Pwani yameilaumu serikali kwa kuhusika moja kwa moja na kashfa za ufisadi, hatua inayohujumu maendeleo.

Mashirika hayo yakiongozwa na shirika la Haki Afrika, yamesema kuwa iwapo serikali haitajitokeza wazi wazi na kuwakabili maafisa na viongozi fisadi serikalini basi taifa litadidimia pakubwa kiuchumi.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumapili, afisa wa haki na sheria katika shirika la Haki Afrika Francis Auma amesema kuwa ipo haja ya viongozi wafisadi kujiuzulu mara moja na kupeana nafasi ya uchunguzi kwani ni aibu kubwa kwa taifa.

“Tunawaambia viongozi wote wanaokabiliwa na kashfa za ufasidi kujiuzulu madarakani na kuchunguzwa kwani wamezoea kunyakua mali ya umma na kukandamiza baadhi ya idara ili kujinufaisha kibinafsi," alisema Auma. 

"Sisi kama mashirika ya kijamii hatutakubali kuona taifa hili likididimia kutokana na uongozi duni wa wakiimla na kidikteta," aliongeza Auma.

Naye mkurugenzi wa Shirika la Wanawake na Maendeleo eneo la pwani Betty Sharon amesema kuwa iwapo Rais Uhuru Kenyatta atashindwa kukabiliana na sakata hizo nchini basi serikali yake itakuwa imedhihirishwa wazi kuwa imeshindwa na uongozi.

“Tunamuomba kiongozi wa taifa kuibuka na mbinu mbadala za kudhibiti ufisadi nchini na maafisa na viongozi wafisadi wafungwe gerezani kwa kuhujumu mali ya umma," alisema Sharon.

Mashirika hayo ya kijamii yameahidi kuzuru mashinani na kuhamasisha jamii jinsi ya kuwatambua na kuwashtaki maafisa na viongozi fisadi ili kulinda mali ya umma.