Vijana wanaopata riziki yao kwa kuzoa mipira na kontena za plastiki katika jaa la Kibuyuni wametoa hofu ya kupoteza ajira iwapo jaa hilo litaondolewa.
Haya yanajiri baada ya wakazi wa eneo la Kibuyuni katika mtaa wa Likoni, Kaunti ya Mombasa, kutoa shinikizo la kutaka jaa hilo kuondolewa.
Vijana hao walisema kuwa jaa hilo ndilo huwapa mkate wao wa kila siku na wengi wao wana familia za kuwategemea.
Vijana hao wameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kutafuta namna ya kuwapa ajira mbadala ya kujimudu huku wakazi wakiaapa kusimamisha utupaji taka katika eneo hilo iwapo serikali ya Kaunti itachelea kufanya hivyo.
Wakiongozwa na John Gatheri na Alfred Mwombe kwenye mahojiano siku ya Jumatano katika eneo hilo, vijana hao walisema kuwa japokuwa kuna uhalali wa wakazi kulalamikia uwepo wa jaa hilo na harufu mbaya, wangependekeza jaa hilo libaki mahali hapo, lakini kitengo cha kuzoa taka kutoka kaunti hiyo kuwajibikia uzoaji taka kila baada ya siku tatu ili kuepusha mrundikano wa taka.
“Wengine wetu tuna familia na tunalipa kodi ya nyumba kupitia kwa kazi hii ya kuzoa plastiki ambazo mara nyingi tunawauzia vijana wa kuuza sharubati, na nyingine tunawapelekea watu wa uzani ambao hutulipa kwa kiwango za uzani cha chupa hizo ambazo tunawasilisha kwao,” alisema Gatheri.
Vile vile vijana wengine ambao hukusanya mabaki ya vyakula na kuwauzia wavuvi baharini kama chambo cha samaki, waliunga mkono kauli ya Gatheri na kusihi serikali ya Kaunti kuweka hela za kuwafadhili kupitia miradi ili nao waendelee kujimudi kimaisha iwapo jaa hilo litaondolewa.