Wabunge wote tisa katika kaunti ya Kisii wameombwa kueleza wazi jinsi pesa za hazina ya ustawi maeneo bunge CDF zimetumika katika maeneo bunge yao na ni miradi ipi zimefanya tangu mwaka wa 2013.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa tangu serikali za ugatuzi zianzishwe nchini, wabunge hawajaonekana kuzitumia pesa hizo za CDF kuleta maendeleo.
Akizungumza siku ya Jumanne mjini Kisii, mwenyekiti wa chama cha kutetea haki za kibinadamu katika kaunti ya Kisii Vincent Gekonge aliomba wabunge kueleza wazi pesa za CDF zimefanya nini katika kaunti hiyo.
Kulingana naye, serikali ya kaunti hiyo ndio imefanya miradi mingi, huku chochote kikihitajika kufanywa serikali ya kaunti ndio hulaumiwa zaidi ikilanginishwa na serikali ya kitaifa haswa wabunge.
“Naomba wabunge wote tisa wa kaunti ya Kisii waeleze miradi ya maendeleo wamefanya kupitia hazina ya CDF,” alisema Gekonge.
“Wabunge hawa hawajafanya chochote maana barabara zile zinastahili kutengenezwa na serikali ya kitaifa hasijafanywa hadi sasa kazi yao ni gani ? tunaomba watueleze ,” aliongeza Gekonge.
Gekonge alidai kuwa wabunge hao hutumia pesa hizo za CDF kujinufaisha wao wenyewe kando na kusahau kutekeleza majukumu mengine ya wakazi.