Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wamiliki wa biashara ndogo ndogo mjini Mombasa wanapanga kuandamana iwapo serikali ya kaunti haitachukua hatua na kuwakomesha maafisa wake dhidi ya ulaji rushwa.

Wakizungumza siku ya Jumanne mjini humo, wafanyibiashara hao, ambao wengi wao hufanya biashara karibu na Hospitali ya Mkoa ya Mombasa, walidai kuwa maafisa wa mji huwalazimu kuwapa hongo na hata kuchukua chakula kutoka kwao bila kulipa.

Michael Mutinda, mfanyibiashara katika eneo hilo alidai kuwa maafisa hao huchukua shilingi 200 na matunda ya shilingi 50 kutoka kwake kila siku kama hongo.

Kauli yake iliungwa mkono na mwenzake Hussein Ali, anayefanya biashara ya kuuza mayai.

Ali alidai kuwa anapanga kufunga biashara yake kwani faida anayopata huishia kwa maafisa hao.

Wafanyabiashara hao sasa wameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuwachukulia hatua maafisa hao la sivyo wataandamana.

Mwezi Desemba 2015, Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho, aliwaonya maafisa wa mji dhidi ya ulaji rushwa kufuatia malalamishi kutoka kwa wakaazi.