Mwenyekiti wa usajili wa wapiga kura katika eneo la Nyanza kusini Sarah Ogaro amewashauri wakaazi kuacha tabia ya kusubiri hadi nyakati za mwisho ili kujitokeza kujiandikisha kama wapiga kura.
Kulingana naye kuna idadi kubwa ya watu ambao hukawia kuchukua kura nao husubiri hadi nyakati za mwisho kufika, jambo ambalo hutatiza shughuli hiyo.
Akizungumza siku ya Jumatano katika eneo bunge la Bochari, Ogaro alisema wale ambao bado hawajajisali kama wapiga kura wajisajili kabla ya tarehe 15 mwezi huu.
“Tarehe 15 shughuli ya usajili itafika mwisho na ninaomba wale ambao hawajapata kadi ya kura wafike kwa vituo vya usajili ili kujiandikisha,” alisema Ogaro.
Wakati huo huo, mwenyekiti wa chama cha Maendeleo ya Wanawake katika kaunti ya kisii Bethsheba Sanaya aliwahimiza akina mama kujitokeza kwa wingi ili kujisajili kama wapiga kura kubadilisha uongozi.
“Sisi akina mama na vijana wengine wa kike tuko wengi zaidi katika taifa la Kenya," alisema Sanaya.
"Naomba tupate kura ili tuchague viongozi hasa akina mama ambao watatuwakilisha katika serikali kwa kuleta maendeleo,” aliongeza Sanaya.