Wazazi kutoka Njoro, Kaunti ya Nakuru, wamelalamikia ongezeko la wasichana wadogo wanaojihusisha na ukahaba.
Wakizungumza siku ya Jumatano wakiongozwa na Joseph Kirui, wazazi hao waliwataka machifu na maafisa wa polisi eneo hilo kufanya upelelezi na kunasa wazazi wa wanafunzi watakaopatikana kwenye vyumba vya burudani wakijihusisha na anasa wakati huu wa likizo.
“Wanafunzi wengi wa darasa la nane wanauza miili yao ili wapate pesa ya kununua vipodozi,” alisema Kirui.
Jane Wambui, mkazi wa eneo hilo, alidai kuwa visa vya maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi vimeripotiwa kuongezeka kutokana na kukidhiri kwa biashara hiyo haswa nyakati za usiku katika maeneo ya kibiashara ya Mauche, Likia, Mau-Narok na Ndeffo.
“Tungetaka serikali iingilie kati kwa sababu wengi wa watoto hao hawana hata vitambulisho kwani wako chini ya miaka 18,” alisema Wambui.
Kirui aidha alidai kuwa baadhi ya maafisa wa polisi huwakamata wanafunzi hao na kisha kuwaachilia baada ya kupewa mlungula.