Wanafunzi wa kata ya Bogusero Kaskazini, eneo bunge la Kitutu Chache Kusini wameonywa dhidi ya kukesha katika sherehe za usiku kama vile mazishi.
Akizungumza siku ya Alhamisi, Chifu wa eneo hilo Francis Marigimarigi alidokeza kuwa onyo hilo ni miongoni mwa kampeni za kuhakikisha kuwa viwango vya elimu katika eneo la Bogusero vinaimarika.
“Hii ni sheria ambayo tumeweka tukishirikiana na wazee wa vijiji ili kusaka na kuwachukulia hatua wanafunzi ambao hukesha katika hafla wakati ambapo wanastahili kuwa nyumbani," alisema Marigimarigi.
Aliongeza, "Iwapo kuna mwanafunzi ambaye atapatikana wakati wa msako tutamcharaza viboko, kisha baadaye mzazi wake atueleze alikuwa wapi wakati mtoto alitoka nje usiku."
Vilevile, chifu huyo amewataka wazazi kuwa macho na kuhakikisha kwamba watoto wao hawahudhurii hafla hizo, kwani visa hivyo ndivyo huchangia wanafunzi kulala darasani.
“Watoto wanalala darasani kwasababu wanakesha kwenye matanga usiku kucha. Hivyo basi, wazazi wote wahakikishe kwamba watoto wao wanalala nyumbani kwasababu nikisikia habari yoyote kama hiyo, nitawaita askari jamii ili tuwakamate watoto hao,” aliongeza Marigimarigi.
Chifu huyo amewaomba wazazi kushirikiana na viongozi wa serikali ili kukomesha visa hivyo.