Wakazi wa eneo la Ogembo Kaunti ya Kisii wanaitaka serikali ya kaunti kuwajengea kituo kipya cha magari baada ya ajali mbaya kutokea siku ya Jumapili.
Wakazi hao walisema kwamba stegi hio imetengewa mahali hatari karibu na barabara kuu ya kutoka Kisii Kuelekea Kilgoris. Wanataka stegi hiyo kuhamishiwa mahali palipo na usalama zaidi.
Wakiongonzwa na mmoja wa viongozi wa steji Charles Makoyo pindi tu baada ya ajali hiyo ambapo watu wanne walipoteza maisha, wakazi hao walisema kuwa ajali nyingi zimetoea mahali hapo.
“Ajali nyingi zimetokea hapa kwa sababu ya hii steji kuwa karibu na barabara sana, watu wengi wamepoteza maisha yao hapa. Hatutaki jambo hili liendelee,” alisema Makoyo.
Kituo hicho cha magari kinatumiwa na wahudumu wa matatu, teksi na bodaboda.
Makoyo aliilaumu serikali ya kaunti kwa kuzembea katika kazi yake ya kuwahakikishia wenyeji usalama barabarani, jambo ambalo anasema wameahidiwa kwa muda. Alisema kuwa ikiwa suala hio halitashughulukiwa kwa dharura wakazi watafanya maandamano.
"Tunaiomba serikali ya Gavana James Ongwae kutujengea steji mahali tofauti na iwapo hatafanya haraka tutaongoza watu kufanya maandamano kutoka hapa Ogembo hadi mjini Kisii," kiongozi huyo wa steji alisema.
Baadhi ya abiria ambao walishuhudia ajali hiyo ya jana adhuhuri waliwashutumu wahudumu wa matatu kwa kutowajibika. Walisema kuwa wengi wao hawaegeshi magari yao vyema wakizingatia udogo wa kituo hicho.