Maafisa wa polisi kaunti ya Kisii wamesema wameimarisha usalama mjini Kisii wakati maonyesho ya kilimo yanaendelea.
Kamanda wa polisi Simon Kiragu siku ya Jumatano alisema kuwa usalama ungeimarishwa vya kutosha katika mji wa Kisii kufuatia na maonyesho ya Kilimo ambayo yalianza siku ya Alhamisi.
Maonyesho hayo yatakamilika siku ya Jumapili tarehe 12 mwezi wa Julai.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kisii alisema polisi watashika doria mjini hadi mwisho wa monyesho hayo na kuomba wakazi wawe na imani na polisi na kuripoti jambo lolote lislo la kawaida bila kusita.
“Ninawahakikishia wakazi wa Kisii kwamba mji huu ni salama, wasiwe na wasiwasi kwenda kutazama maonyesho ya kilimo. Kama kuna visa vyovyote nawaomba wasisite kuripoti,” mkuu huyo wa polisi alisema.
“Usalama umeimarishwa katika uwanja wa gusii ambapo maonyesho hayo yatafanyiwa na mji wote wa Kisii kwa jumla,” aliongeza.
Maonyesho ya kilimo hufanyika kila mwaka katika kaunti ya Kisii ambayo hufunza watu mbinu za ukulima wa mimea pamoja na ufugaji. Visa vya utovu wa usalama na utapeli huripotiwa wakati kama huu ambapo wakazi kutoka sehemu mbalimbali za kaunti hukusanyika mjini.