Share news tips with us here at Hivisasa

Jamii ya Ogiek katika kaunti ya Nakuru imetakiwa kujihusisha kikamilifu katika shuguli za maendeleo iwapo inataka kunufaika na ugatuzi.

Mwakilishi wadi ya Tinet David Sitienei Malel amesema kuwa itakuwa vigumu kwa jamii hiyo kunufaika na kufurahia matunda ya ugatuzi iwapo haitajitokeza na kujihusisha na shughuli za kisiasa na maendeleo.

Akizungumuza afisini mwake alhamisi, Malel alisema kuwa jamii ya Ogiek ina uwezo mkubwa unaoweza kutumika katika kubadilisha maisha yao na kuwa kama jamii zingine.

“Jamii ya Ogiek imelalamika kwa muda mrefu kuwa imetengwa lakini ni wakati wao na jukumu lao kujitokeza sasa na kung’ang’ania kilicho chao katika utawala wa kaunti kwa sababu hatuwezi kuendelea kukaa tukingoja tuletewe na wengine,” alisema mwakilishi huyo wa wadi.

Malel sasa anawataka watu kutoka jamii hiyo kujitokeza nakupigania nyadhifa za uongozi pamoja na kutafuta kazi katika serikali ya kaunti.

“Katiba inawaruhusu wakenya wote wakiwemo Ogiek kupigania uongozi katika ngazi mbalimbali na mimi nawataka wajitokeze na hata kutafuta kazi katika serikali ya kaunti kama wanataka kujiendeleza kimaisha,” alisema.

Kiongozi huyo alisema kuwa mabadiliko ya maisha katika jamii ya Ogiek yataletwa na watu wa jamii hiyo wenyewe bali siyo watu wa nje.

“Huu ugatuzi ni wa kila mkenya na kila mkenya anapaswa kufurahia matunda yake lakini tukilala, hatuwezi kufurahia matunda hayo,” alisema.