Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho, amewahimiza wakaazi wa Mombasa kuchukua vitambulisho kwa wingi, ili kujiandaa kupiga kura kwa wingi kwenye chama cha upinzani katika uchanguzi mkuu ujao.
Akiongea katika jiji la Mombasa kwenye hafla ya kuzindua barabara ya Fidel, Gavana Joho alisema kuwa sharti wakaazi wa eneo la Pwani kujiandikisha kama wapiga kura kwa idadi kubwa na wale ambao hawana vitambulisho kuhakikisha kuwa wamepata hati hizo muhimu.
“Hakikisha kuwa mnajiandikisha kwa wingi ndio tuwe na ushindi ifikapo mwaka wa 2017 kwa chama chetu cha upinzani,” alisema Joho.
Wakaazi ambao walikuwa katika hafla hiyo walimwahakikishia gavana na kiongozi wa upinzani kuwa wapo tayari kujiandikisha kupata vitambulisho rasmi, ili kuona kuwa wananyakua uongozi kupitia chama hicho cha upinzani.
“Tuko tayari kujiandikisha ili kushinda uchaguzi mkuu ujao. Tayari tumeanza kuwahimiza vijana wengine ambao wamefikisha umri wa kupata vitambulisho kuanza kufanya hivyo. Tupo tayari kwenye siasa za mwaka wa 2017,” alisema Joe Murima.
Kiongozi wa muungano wa Cord Raila Odinga anatarajiwa kufanya ziara yake kwenye eneo la Pwani, huku akitarajiwa kuelekea Malindi siku ya Alhamisi kwenye kampeni rasmi ya atakayepeperusha bendera ya Cord kwenye kiti cha ubunge cha Malindi.