Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Visa vya magonjwa yanayotokana na utumiaji wa maji machafu katika Kaunti ya Mombasa miongoni mwa wanafunzi vinatarajiwa kupungua kwa kiasi kikubwa.

Hii ni baada ya Serikali ya Kaunti ya Mombasa ikishirikiana na ile ya Uholanzi, kufungua rasmi mradi wa maji safi na vyoo vya kisasa katika Shule ya msingi ya Mrima, eneo la Likoni.

Akiwahutubia wakaazi wa eneo hilo siku ya Alhamisi, Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho alisema kuwa mradi huo utafikia shule zote za msingi katika kaunti hiyo, ili kuhakikisha kuwa elimu bora na usafi kwa watoto wa shule za umma katika kaunti hiyo unazingatiwa.

"Tutahakikisha kuwa maradhi ya kiafya yanayowakumba watoto wetu tumeyazuia kwa kuzingatia usafi na mazingira bora, kwani tumeanzisha elimu ya kudumisha usafi kwa wanafunzi na walimu pia, kuhakikisha kuwa elimu bora inaendelezwa,” alisema Joho.

Wakati huo huo amewataka wakaazi wa Shamba la Waitiki kutolipa ada ya shilingi elfu 182 kama ilivyopendekezwa na serikali kuu, akisema kuwa ni ukiukaji wa haki za Wakenya.

Aidha, aliwahimiza wakaazi wa eneo hilo kuhakikisha kuwa wanajisaliwa kama wapiga kura ili kuchagua viongozi waadilifu.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Balozi wa Uholanzi humu nchini Francis Maken, Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko, Mkuu wa Idara ya Mazingira na raslimali za maji Kaunti ya Mombasa Bi Fatma Awadh, pamoja na viongozi wengine.