Meneja wa kampuni ya Rumish Hardware iliyoteketea hivi maajuzi kwenye mkasa wa moto mjini Nakuru ametoa wito kwa serikali ya kaunti kuboresha mbinu zao za kukabiliana na majanga mjini na hasaa majanga ya moto.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne mjini Nakuru, Tom Kibisu alisema kuwa ingawa wazima moto walifika wakati ambapo duka lao lilikuwa likiteketea, walichukua mda na juhudi zao hazikufikia kiwango cha matarajio yao.
"Uongozi wa kaunti sasa unatakikana kutia juhudi katika kukabiliana na majanga mbalimbali. Ingawa walifika kutusaidia kukabiliana na moto, msaada huo haukutosha ingawa walijitahidi kadri ya uwezo wao. Tunataka gavana Kinuthia Mbugua atilie maanani haswaa katika kitengo cha kuzima moto," alisema Kibisu.
Kibisu anasema kuwa ingawa moto uliozuka uliwaathiri kibiashara, bado wana mpango wa kurudi katika jumba lile.
Hata hivyo, anasema kwa sasa biashara yao inaendelea katika kijimba kilicho kando na jumba hilo lililoathiriwa na moto.
Kwa upande wake afisaa mkuu wa idara ya moto katika kaunti ya Nakuru Joseph Kuria, uwezo wao wa kufika mahali ambapo wameitwa na kudhibiti moto hutegemea upesi wa wananchi kuwaita.