Share news tips with us here at Hivisasa

Muungano wa wauguzi nchini KNUN, tawi la Nyamira umesema huenda ukalazimika kuitisha mgomo wa wanachama wake iwapo serikali ya kaunti hiyo haitochukua hatua za haraka kuajiri wahudumu zaidi wa afya.

Akihutubia wanahabari siku ya Jumatatu, katibu wa chama hicho tawi la Nyamira Richard Oruta, alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo inastahili kushughulikia kwa haraka hali ya kutokuwepo wahudumu wa afya wakutosha kwenye hospitali na zahanati nyingi katika kaunti hiyo.

Oruta alisema kuwa wahudumu wengi wa afya hulazimika kufanya kazi kwa masaa mengi kutokana na changamoto hiyo.

"Ni jambo la kushangaza kwamba baadhi ya wahudumu wa afya ambao ni wanachama wetu hufanya kazi nyingi kuliko ilivyo kawaida, ikizingatiwa kwamba masharti ya kazi hayajaweka wazi suala hilo," alisema Oruta.

Hata hivyo, Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama aliyekuwa akiwahutubia wahudumu zaidi ya 220 walioajiriwa na serikali ya kaunti hiyo siku ya Ijumaa wiki jana kule Kebirigo, alisema kuwa serikali yake itaweka mikakati ya kuhakikisha kuwa suala la kutokuwepo kwa wahudumu wakutosha linaangaziwa.

"Ninafahamu kwamba tuna ukosefu wa wahudumu wa afya wa kutosha kwenye hospitali na zahanati zetu ila serikali yangu imeweka mikakati ya kuhakikisha tumeajiri wahudumu zaidi. Tayari tumeajiri wahudumu 220 watakaosaidia kuziba pengo hilo," alisema Nyagarama.