Waziri wa elimu nchini Fred Matiang'i ametishia kuvunjilia mbali bodi za shule za umma zinazoingisha siasa za ukabila kwenye usimamizi wa shule ikizingatiwa hali hiyo huathiri viwango vya masomo kwenye shule nyingi nchini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu kwenye mkutano wa washikadao kule Kebirigo kaunti ya Nyamira siku ya Ijumaa,  Matiang'i alisema itamlazimu kuzivunja bodi za aina hiyo kama njia mojawapo ya kuzisaidia shule kuimarika kimasomo. 

"Haya mambo ya bodi za shule za umma kuwa na mazoea ya kuingisha siasa kwenye usimamizi wa shule kamwe haitovumiliwa. Inawezekana aje kwamba watu wanaweza mkataa mwalimu mkuu wa shule eti kwa kuwa sio wa kabila lao," aliulixa Matiang'i.

Matiang'i aidha aliwaonya walimu wakuu wa shule za msingi wanaoathiri ratiba za masomo shuleni kwa kutumia uwanja wa shule kama sehemu za kuandaa hafla za mazishi na michango, hali ambayo alisema huathiri kumalizika kwa silabasi kwa wakati ufaao.

"Nimekuja kugundua kuwa baadhi ya ratiba za masomo kwenye shule nyingi za umma humu nchini huathiriwa pakubwa kutokana na walimu wakuu wa shule hizo kuruhusu uwanja wa shule kutumiwa kama sehemu za kuandaa sherehe za mazishi, lakini yeyote anayeruhusu hayo wacha afahamu kwamba hatuko tayari kufanya kazi naye," alionya Matiang'i.