Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Bi Mishi Mboko ameitaka serikali ya kaunti kununua magari ya ambulensi zitakazo saidia katika utoaji wa huduma za kiafya katika eneo la Likoni.

Mboko alisema kuwa eneo la Likoni liko na ambulensi moja pekee, hali ambayo imekuwa changamoto kubwa kwa wakaazi hao, ikizingatiwa kuwa idadi ya wakaazi katika eneo hilo imeongezeka.

Akihutubia wakaazi wa eneo hilo katika shule ya msingi ya Mrima siku ya Alhamisi, Mboko alisema kuwa iwapo serikali ya kaunti hiyo itazingatia suala hilo, basi kwa kiwango kikubwa itawasadia akina mama wajawazito katika kuvuka kivuko cha feri wakati wa dhararu.

"Tuiomba serikali ya kaunti ya Mombasa chini ya Gavana Joho kuhakikisha kuwa inanunua magari ya ambulensi zitakazotoa huduma katika eneo la Likoni ili kusaidia wakati wa dhararu na kupunguza changamoto katika kivuko cha feri,” alisema Mboko.

Wakati uo huo, aliwakashifu wanasiasa waliokihama chama cha ODM, kwa kusema kuwa kamwe viongozi hao hawatayumbisha chama hicho.

Mboko aliahidi kumuunga mkono Gavana Joho katika juhudi zake za kuimarisha chama.

"Wale viongozi waliotangaza kukihama chama cha ODM wajue kwamba chama hicho hakitayumbishwa na mtu yoyote, kwani sisi tuko nga'angari,” aliongeza Mboko.