Mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire amewaomba watu wanaoishi na ulemavu kutoka eneo bunge lake kujiandikisha kupokea pesa za basari.
Akihutubu katika eneo la kibiashara la Manga siku ya Jumatatu, Bosire alisema kuwa watu wanaoishi na ulemavu wana haki ya kupata ufadhili wa kimasomo kama watu wengine, akihoji kuwa kuna haja ya watu kama hao kuimarisha maisha yao.
"Eneo bunge letu lina orodha ya watu wanaoishi na ulemavu na kile ambacho tunaweza fanya ili kuwasaidia ni kuhakikisha kuwa tunawapa ufadhili wa kifedha kutoka kwenye hazina ya maendeleo bunge ili kuwasaidia kuimarika kimasomo," alisema Bosire.
Bosire aidha aliipa changamoto serikali ya kaunti ya Nyamira kutenga pesa za kuwafadhili watu wanaoishi na ulemavu, akisema kuwa serikali ya kaunti ya Narok imewatengea watoto walemavu katika kaunti hiyo shillingi millioni 60, ilhali kaunti ya Nyamira haijafuata mkondo huo.
“Ninaiomba serikali ya kaunti hii kuhakikisha kuwa imetenga pesa za kuwafadhili watoto walemavu, kwa kuwa kaunti zingine kama ile ya Narok tayari imetenga shillingi millioni 60 kwa watoto walemavu," alisema Bosire.
Mbunge huyo aidha alisema kuwa tayari eneo bunge lake limebuni kamati teule itakayoangalia na kushughulikia maslahi ya watu wanaoishi ma ulemavu.