Huku usajili wa wapiga kura ukiendelea kote nchini wakazi wa wadi ya Sensi eneo Bunge la Kitutu Chache Kaskazini kaunti ya Kisii wameshauriwa kutokubali kuhamishwa kwa wadi zingine ili kusajiliwa kama wapiga kura.
Ushauri huo umetolewa baada ya kubainika kuwa kuna baadhi ya wanasiasa ambao wanahamisha wakazi wa wadi hiyo hadi wadi zingine zilizoko karibu ili kusajiliwa kama wapiga kura.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika wadi hiyo ya Sensi mwanasiasa alinaye pania kuwania kiti hicho cha uakilishi wadi katika wadi hiyo Evans Toeri aliwashauri wakazi hao kutokubali kupelekwa wadi zingine kwani hawatapata uhuru wa kuchagua viongozi wanaowahitaji katika maeneo yao.
Mwanasiasa huyo alidai kuwa kuna wanasiasa ambao huwadanganya wakazi hao kwa kuwanunua kwa shillingi 1,000 ili kusajiliwa katika wadi tofauti kando na ile waliokuwa wakaazi.
“Naomba wakazi wa wadi hii ikiwa mnahitaji kuwachagua viongozi wa maenedeleo msikubali kupelekwa kwa wadi zingine kusajiliwa , elfu moja ni kitu kidogo sana naomba kila mkazi kusajiliwa kwa wadi yake ili kuchagua viongozi wanaofaa wa maendeleo,” alisema Toeri.