Mwenyekiti wa muungano wa wazazi nchini (KNAPs) Musau Ndunda amelihimiza bunge kupitisha mswada wa chama cha huduma kwa walimu nchini TSC ili kumpa waziri wa elimu mamlaka ya kuwachukulia hatua walimu wakuu wanaowatoza wazazi karo kinyume na sheria.
Akizungumza na wanahabari mjini Nairobi siku ya Jumatatu, Ndunda, alisema kwa sasa ni vigumu kwa waziri wa elimu Dkt Fred Matiang'i kuwaadhibu baadhi ya walimu wakuu wenye tabia ya kuongeza karo maradufu kwani agizo lake halina nguvu kutokana na kuwa walimu hao wako chini ya TSC.
''Njia ya pekee ya kumaliza huu mgogoro baina ya walimu na wazazi kuhusu nyongeza ya karo ni kumpa mamlaka waziri wa elimu ili anapotoa agizo lolote, kisha agizo hilo likose kufuatwa ana uwezo wa kuwachukulia hatua kali wahusika,'' alisema Ndunda.
Ndunda pia alisema muungano wa wazazi tayari umepata ushahidi wa kutosha unaoonyesha namna zaidi ya shule 100 nchini, baadhi yao zikiwa katika mkoa wa Magharibi zinavyotoza karo zaidi ya ilivyoagizwa na serikali.
''Tumeshapata taarifa zinazoonyehsa jinsi baadhi ya walimu wakuu nchini wanavyowahadaa wazazi kwa kuongeza karo kwa vitu visivyowafaidi wanafunzi,'' alisema Ndunda.
Haya yanajiri wakati serikali kupitia katibu katika wizara ya elimu Belio Kipsang ikiwaagiza wakuu wote wa elimu nchini kuwasilisha ripoti kwa wizara hiyo kuhusu ulipaji karo.
Siku ya Jumatatu, Kipsang aliwataka wakurugenzi wa elimu katika kila kaunti nchini kuwasilisha majina ya shule zilizokiuka mwongozo wa karo uliotolewa na serikali Februari 2015.
Kwa mujibu wa mwongozi huo, wanafunzi katika shule za kutwa wanafaa kulipa Sh9,347, wale wa shule za malazi Sh53,543 huku wanafunzi wenye mahitaji maalum wakilipa Sh37,210.
Hata hivyo kuna madai kuwa baadhi ya shule zimeongeza karo hadi Sh100,000.
Shule zote za umma kote nchini zilifunguliwa siku ya Jumatatu kwa muhula wa kwanza huku wazazi wakilalamikia ongezeko la karo na kupanda kwa bei ya vitabu.